
UZALISHAJI
na ufugaji bora wa sungura kibiashara umewatoa kimasomaso wajasiriamali
waliochangamkia na kuibuka kuwa mwarobaini wa umasikini. Ufugaji wa sungura ni
shughuli ya kiuchumi inayokua kwa kasi kubwa. Sungura huzaliana ndani ya
kipindi cha miezi miwili tu.
Sungura
huzaliana kwa kasi watoto sita hadi 10 kwa mkupuo wa kwanza. Huzaa pia watoto
10 hadi 15 kwa mkupuo wa pili.
Mkurugenzi
wa Tanzania Business Creation Company (TBCC), Elibariki Mchau anasema, ufugaji
wa sungura ni rahisi. Hauhitaji eneo kubwa kwa ajili ya malisho.
Mchau
anasema hayo kwenye kongamano aliloitisha kwa lengo la kutoa mafunzo juu ya
faida za ufugaji wa sungura. Wakala wa Ufugaji wa Sungura Mkoa wa Dodoma,
Angumbwike Ng’wavi anasema, kongamano hilo ni la pili baada ya lililofanyika
Oktoba 8, mwaka jana.
“Kongamano
hili limetupa faida kubwa sisi wakazi wa mkoa wa Dodoma,” anasema Ng’wavi
akisisitiza wameelimisha umuhimu wa kujikita katika uchumi wa kufuga sungura
kibiashara.
Mchau
anasema utafiti uliowahi kufanywa na taasisi moja ya Marekani, unaonesha ili
kupata nyama kilo 150 ya ng’ombe unahitaji ekari mbili za malisho lakini ili
kupata kilo hizo za sungura unahitaji hatua tano kwa tano.
Nyama ya
sungura ipo katika kundi la nyama nyeupe ambayo watu wengi wanashauriwa kula.
Haina lehemu kama ilivyo kwa ng’ombe na mbuzi. Pia haina kemikali hatarishi.
Kutokana na
ubora wa nyama yake, imepata soko kubwa la kupendwa kuliwa duniani kote,
kutokana hasa na kuwa na carolies chache. Inazo 795 ikilinganishwa na kuku
yenye 810, bata mzinga 1,190, kondoo 1,420, ng’ombe na nguruwe 2,015. Ufugaji
wa sungura umepanda chati siyo tu kwa ajili ya nyama, bali pia, mkojo wake
hutumika kama viuatilifu.
Mkojo
ukizimuliwa na maji kwa kuchanganya katika uwiano wa lita tano za mkojo na 20
za maji, inatumika kama mbolea ya kunyunyizia mboga kunusuru mimea hiyo na
wadudu waharibifu.
Wakati
mwingine mchanganyiko huo wa maji na mkojo, unaweza kutumika kunyunyizia kwenye
udongo wakati wa kuandaa ardhi kwa kilimo kwa kuchanganya na udongo kama mbolea
ya majimaji.
Mbolea ya
mnyama huyo ni bora kutokana na mchanganyiko wa madini yaliyomo ambayo
yanafanya ifae zaidi kwa kilimo na kuongeza ubora wa udongo.
Ina
fosiforasi asilimia 87, naitrojeni (2.2), potasiamu (2.30), salfa (36), kasiamu
(1.26) na magnesiamu 40. Mkojo wa sungura tofauti na wanyama wengine, unatajwa
kitaalamu kuwa unaweza kubadilika rangi; njano, kijani, pinki na damu ya mzee.
Hali hiyo
inatokana na mwili wa sungura kutokuwa na asidi, kazi ambayo inafanywa vizuri
na ini pamoja na kongosho kuchuja na kutoka nje.
Mchau
anaelezea pia kichwa cha mnyama huyo kuwa ni dawa muhimu kwao. Kikitengenezwa
supu, inasaidia kuongeza nguvu za kiume.
Sungura wana
soko la uhakika na kubwa nje ya nchi, ambalo pia linawezekana kuwapo Tanzania
kutokana na uhakika wa kampuni yake kuwa mnunuzi mkuu wa nyama yake kutoka kwa
wafugaji.
Mfugaji
anatakiwa kujikita katika kufuga sungura bora ambapo wazazi wake sita ambao ni
dume mmoja na majike sita anapata kutoka kampuni hiyo kwa Sh 85,000 kila mmoja.
TBCC inatoa
mkataba kwa mfugaji ili kuwa na uhakika wa soko la sungura wake. Sungura
waliozalishwa watanunuliwa wakiwa hai kila wanapofika umri wa miezi minne hadi
mitano.
Katika
kurahisisha fursa hiyo, kampuni inatoa mafunzo kwa wafugaji na pia huduma ya
utengenezi wa mabanda yake ya kufugia sungura wazazi na watoto wakizaliwa.
Sungura akifugwa vizuri anakuwa na uzito wa kilo tatu hadi tano, na kampuni
hiyo inanunua kwa Sh 8,000 na kuuzwa kwa masoko mbalimbali likiwamo la Jamhuri
ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Mchau
anasema, ili kufikia uzito mkubwa, lazima atunzwe na alishwe vizuri chakula
bora maalumu chenye virutubisho. Hulishwa majani makavu na mabichi, hupewa
madini, vitamini, maji safi na salama ambayo hayana chumvi au kemikali
hatarishi.
Akilishwa
vizuri, sungura jike anaweza kuzaa mara sita ambapo kila uzao anaweza kuzaa
watoto sita hadi 10 na mara sita ni sawa na kuzaa sungura 36 hadi 60.
Hivyo kwa
jozi moja ya sungura dume mmoja na majike sita, tegemea kupata sungura 216 hadi
360 kwa mwaka, pasipo kuongeza jozi nyingine ya wazazi.
Sungura
hubeba mimba kwa siku kati ya 26 hadi 31, na anatumia saa nne hadi sita kuzaa
watoto alionao tumboni kama ni 10 hadi 15, ambao huzaa mmoja baada ya mwingine.
Kama wanyama
wengine, baada ya kuzaa huwalamba na watoto huanza maisha wakitafuta matiti ya
mama wanyonye. Sungura huzaliwa akiwa hawaoni na hawana manyoya bali huanza
kutoka siku ya kwanza hadi ya tano.
Siku ya
saba, watoto wanaanza kufungua macho na ya 10 wanakuwa na macho maangavu. Baada
ya siku 14 tangu kuzaliwa kwao, na tangu hapo watatoka kwenye kikasha na kula
chochote anachokula mama yao.
Post a Comment